ALAMA ZA PENZI LA KWELI
Mapenzi ni kitu kizuri kwani muanzilishi
ni MUNGU na siku zote MUNGU NI MWEMA. Kuwa na mtu anaekupenda ni
haki yako toka wa MUNGU ALIEKUUMBA na ukiona mtu hakupendi maana yake anapingana
na mpango wa MUNGU katika maisha yako na ni wajibu wako kusimamia haki yako ya
kupendwa kikamilifu.Ni kweli kabisa kuwa unastahili kupendwa kikamilifu ili
uweze kufurahia maisha yako ya kila siku. Toka tukiwa watoto wachanga tunapokea
upendo toka kwa wazazi wetu bila kutoa penzi lolote kwa wazazi wetu lakini kwa
kadri tunavyokua wazazi wetu wanatarajia kuwa tutaweza kushirikiana nao na sisi
kuweza kuchangia katika furaha ya maisha yao. Alama ya kwanza tuionayo kwa
wazazi ni kuhangaikia mahitaji yetu yote jambo ambalo linatupatia afya na
furaha ya kuwemo duniani. Kipindi hichi cha utoto tunakuwa tunategemea wazazi
wetu kwa asilimia 100, yaani hata unapojisaidia mama hata angalia harufu mbaya
bali kwa moyo mweupe ataondoa hali hiyo mbaya. Ili uweze kuwa na penzi la kweli
na uhusiano uliojaa furaha kwa sehemu lazima utajikuta unamtegemea mpenzi
wakoili ufurahia maisha yako. Watu wengi
wanashindwa Kutengeneza mazingira ambapo
penzi tamu linakuwepo kwani pale unapomtegemea mpenzi wako kukujali kwa sehemu
kubwa na yeye akashindwa kukujali unajikuta unaumia japo huwezi kulia kama
mtoto mchanga. UNAPORUHUSU maumivu kuendelea kuongezeka ukubwa moyoni mwako
unahatarisha maisha yako mwenyewe bila kujua.ALAMA zifuatazo zitakusaidia
kuelewa penzi la kweli.
1. KUHESHIMU UHURU WA KUPENDA
Mapenzi ya kweli hayalazimishwi kwani
ni kama vile mzazi halazimishwi kumlisha mtoto wake mwenyewe. Mpenzi mwenye
mapenzi ya kweli atajituma bila kungojea kuombwa au kukumbushwa. Nimekutana na
kesi nyingi ambazo mtu alieachwa na mpenzi wake anataka msaada toka kwangu na
ninapomuuliza mara ya mwisho kumpa zawadi mpenzi wako ni lini, wengi wanasema
juu ya misaada waliyoitoa, “Simu yake iliharibika aliomba Tsh.15,000/=
nilimpatia” nawaambia hiyo sio zawadi huo ni msaada. Zawadi hutokea moyoni na
sio machoni au masikioni, ukiona nguo ya mpenzi wako imechakaa ukamnunulia huo
ni msaada. Mpenzi wako akikuomba pesa aende kutengeneza nywele saloon huo ni
msaada sio zawadi. Zawadi unafikiria moyoni kuwa nikimpatia mpenzi wangu zawadi
ya saa au viatu atafurahi, unanunua na kumpa surprise. Kwa hiyo basi, mtu
mwenye mapenzi ya kweli atajituma yeye mwenyewe kufanya au kusema mambo
yatakayochangia furaha ya mpenzi wake. Kama vili alivyojituma na kukuomba uwe
mpenzi wake anapashwa ajitume katika kufanya mambo yanayokuletea raha.Watu
wengi wana mapenzi toroli, toroli haliwezi kusogea bila kusukumwa kadhalika
watu wenye mapenzi tolroli mpaka waambiwe ndipo wanafanya jambo tamu,
haipendezi iwapo unampenda mpenzi wako.
2. JUHUDI YA KUWA MKWELI
Mtu mwenye mapenzi ya kweli nafsi yake
inafurahia ukweli na hata Biblia inaonyesha hilo, “Upendo haufurahii udhalimu
bali hufurahia pamoja na kweli” (1.WAKORINTHO
13:6). Mpenzi mwenye mapenzi ya kweli atapenda kuwa muwazi kwako na yeye
atataka uwe muwazi kwake. Mpenzi mwenye mapenzi ya kweli atasisitiza ukweli na
hataogopa ukweli japo mara nyingine ukweli unaumiza. Katika kusisitiza ukweli
na uwazi ni sehemu muhimu, ukimboa atakuambia, ukishindwa kumridhisha au
kumfurahisha katika ngoma ya wakubwa au katika maongezi yenu atakuambia
akitegemea utafanya juhudi kuleta mabadiliko. Simu yake itakuwa kama kitabu
kilicho wazi kwako na simu yako atapenda ajue yaliomo.UKWELI utaonekana katika
kutimiza ahadi zake, katika nafasi anayotoa ya kukuthibitishia kuwa anakupenda
na katika kuonyesha hisia zake na mitazamo yake.
3. UNYENYEKEVU WA KWELI
Mpenzi wa kweli anajua mwanadamu
yoyote hukosea na ni mwepesi katika kukubali na kukiri makosa yake bila
kujitetea tetea na kujiinua. Biblia inasema “Vivyo hivyo vijana watiini wazee;
Naam, ninyi nyote jifunzeni unyenyekevu mpate kuhudumiana, kwa sababu Mungu
huwapinga wenye kiburi lakini huwapa Neema wanyenyekevu” (1
PETRO 5:5). Mpenzi wa kweli amelenga kumfurahisha mpenzi wake na hivyo
anapomuumiza au kumkosesha raha mpenzi wake, nafsi yake inajisikia vibaya na
hivyo anakuwa mwepesi kuomba msamaha. Na sio hilo tu bali pia ataonyesha nia na
bidii ya kutokurudia kosa lolote linalomuumiza mpenzi wake.UTAONA aanatafuta
njia mbalimbali za kuweza kukufurahisha bila kujali hisia zake kama BWANA YESU
alivyofundisha kwa kusema “Atakae kuwa
mkubwa miongoni mwenu awe mtumishi wa wote” angalia ukosefu wa unyenyekevu toka
kwa mwanamke kama baba mmoja alivonielezea kwa SMS ‘DR LOVE, MIMI NIKO NDANI YA
NDOA MWAKA WA 4 mke wangu amekuwa mzigo kwangu maana analoliwaze yeye ndo
anataka lifanyike na mara nyingi ameleta hasara katika miradi yetu. NIFANYEJE
ABADILIKE?’’ .UNYENYEKEVU NI KIGEZO MUHIMU SANA KATIKA KUJENGA PENZI LA KWELI.
4. ANATHAMINI NGUVU YA UWEPO WAKE
Bila shaka umeshawahi kuona mtoto wa miaka
miwili au mitatu akimlilia mama yake pale anapoondoka kwenda kazini au
anapotoka kwenda mbali na nyumbani. Ni dhahiri hata wewe katika historia ya
utoto wako ulilia pale mama alipoondoka nyumbani jambo ambalo linashuhudia
umuhimu wa uwepo wa mtu umpendae. Mpenzi wa kweli atajitahidi apate muda wa
kukaa na wewe na kuwa na wewe kikamilifu. Nakumbuka secretary wangu kuniambia
“Doctor na wewe unamzoeza vibaya mke wako, yaani anajua muda wako wa kurudi
nyumbani na sijakuona hata maramoja unachelewa au ukitoka hapa kwenda sehemu
nyingine” nikamwambia kuwa nampenda mke wangu na hivyo kumuona na kuongea nae
ni sherehe kwangu. Mara nyingine baada ya kula napatwa na usingizi lakini kwa
kuwa najua umuhimu wa kukaa na mke wangu sebuleni nitatafuta kitu cha kuchekesha
na tukianza kucheka usingizi unapotea na tunaweza kuongea hadi saa 6 usiku. Ni
muhimu sana kwa wapendanao kupata nafasi ya kukaa pamoja na kucheka pamoja
kwani inaimarisha hisia za kimapenzi kwa umpendae. Ukiona mpenzi wako hathamini
muda wa wewe na yeye kukaa pamoja tambua una mpenzi feki.Mpenzi wa kweli
atahakikisha kuwa kuwepo kwake na wewe ni sehemu ya burudani katika uhusiano wenu.
5. HAOGOPI
Alama muhimu na ya ajabu ya mpenzi wa
kweli ni kwamba haogopi kukuambia ukweli wote na haogopi kukosana na marafiki
zake na hata ndugu zake kwa ajili yako wewe. Mfano mzuri tunaupata toka kwa
Bwana Yesu, “Wakwamwendea mama yake na ndugu zake; wasiweze kumkaribia kwa
sababu ya mkutano. Aakaletewa habari akaambiwa; mama yako na ndugu zako
wamesimama nje wakitaka kuonana na wewe. Yesu akajibu akasema, Mama
yangu na ndugu zangu ndio hawa wananosikiliza neno la Mungu na kulitenda”
(LUKA 8:19-21). Kwa mfano huo
tunaona ni jinsi gani mtu anavyothamini uhusiano wake na mtu ampendae kiasi
haogopi wazazi wake na ndugu zake watasemaje au kujisikiaje. Iwapo unataka
penzi la kweli usifanye maamuzi au uchaguzi unaoongozwa na hofu ya mtu au watu.
Usiogope kumhoji mpenzi wako kwani kwa kumhoji ndio utaweza kupima penzi lake
kwako, je atakusikiliza na kufanya mabadiliko au atakuwa mkatili asiejali hisia
zako? Usimuone mpenzi wako kama jambazi linalo
kulazimisha ufanye mambo yanayotia nafsi yako hasara. Jambazi halijali
hisia zako pale linapopora mali zako zenye gharama kubwa na kukuachia hasara
kubwa sana na mara nyingine hata kukujeruhi vibaya. Mpenzi asiejali hisia zako
hana tofauti na jambazi, hakikisha una mpenzi alie rafiki kwako na sio jambazi.
Mpenzi wa kweli lazima atakupa kipaumbele bila kujali watu au hata nafsi yake
mwenyewe.
6. ANAJITAHIDI KUKUELEWA
Chanzo kikubwa katika mahusiano ya
kimahaba kuingia katika hali ya migogoro ni mmoja kudhania ya kwamba mpenzi
wake ataridhika na penzi analotoa bila kutafuta njia ya kupata uhakika wa
mtazamo huo.
Haijalishi
mpenzi wako anakupenda kiasi gani mtazamo wako hauwezi kuwa mtazamo wake katika
kila jambo. Lazima utambue nyinyi ni watu wawili tofauti na wenye historia
tofauti japo yapo mambo machache ambayo mtakuwa sawa katika mitazamo. Mpenzi
mwenye mapenzi ya kweli atatafuta kuelewa mtazamo wako kwanza kabla hajataka
uelewe mtazamo wake kwanza, atauliza maswali ili apate kuelewa mtazamo wako
bila kukuhukumu. Pale ambapo atapata shida ya kukuelewa ataoyesha kwanini
anapata shida kukuelewa na kukupa kazi ya kufafanua mambo vizuri. Mpenzi wa
kweli hatakuwa mwepesi kusema “Achana na hayo” bali atapenda umueleweshe kabla
hajafanya uamuzi wa kukubaliana na wewe. Huko sio ubishi bali ni kiu ya kupenda
kuelewa ili awe na amani na wewe.
Katika mazingira kama hayo kila mmoja anajitahidi afahamu mahitaji ya
mwingine na kufanya kazi ya kuendelea kumdhibitishia mpenzi wake kuwa bado ni
wa muhimu sana. Katika mazingira ya uwazi na ukweli kila mmoja anajisikia kuwa
anasikilizwa na kueleweka na hisia zake kuheshimiwa. Uonapo mpenzi wako
hakusikilizi au anadharau hisia zako lazima uhusiano wenu utadhurika, je
utajuaje kama mpenzi wako anakupenda iwapo hataki kukusikiliza? Utajuaje kama
mpenzi wako anakupenda iwapo hajali hisia zako? Utajuaje kama mpenzi wako
anakupenda kama hakuhurumii? Utajuaje kama mpenzi wako anakupenda iwapo
hakujali? Utajuaje kama mpenzi wako anakupenda iwapo hakusaidii unapokuwa na
shida, hakulindi dhidi ya vicheche wanaokunyemelea au ndugu wanaowachonganisha,
hakujali unapokuwa na huzuni, hakutii moyo unapokuwa umekata tamaa, haombi
radhi anapokuwa amekosea au hakubembelezi au kukupa zawadi za hapa na pale,.JE
anapokuambia anakupenda anamaanisha nini? Ni kweli kila mmoja ana mapungufu
yake lakini ni muhimu usisitize penzi la
kweli na llenye furaha .
7. TENDO LA NDOA LINAPEWA KIPAUMBELE
Tendo la ndoa ni la kipekee kabisa
katika uhusiano wa kimahaba, eneo ambalo marafiki na ndugu hawaruhusiwi kabisa
kufika au kusogelea. Kutokana na upekee wake huo tendo la ndoa ni kiungo cha
kipekee na muhimu kwa uhai wa uhusiano wa kimapenzi. Tafiti zinaoyesha iwapo
tendo la ndoa (Ngoma ya wakubwa) linaenda vizuri litachangia furaha na ubora wa
uhusiano kwa asilimia kati ya 15 – 20, lakini tendo hilo lisipokuwa na utamu
toshelevu litachangia asilimia 80 – 85 ya migogoro inayojitokeza miongoni mwa
wapendanao. Tendo la ndoa linapunguza makali ya vichocheo(Hormones)
vinavyosababisha hasira. Pale mtu anapofika kileleni kichocheo cha OXYTOCIN
humiminwa kwa wingi na kufanya mtu ajisikie amani katika mwili na nafsi yake.
OXYTOCIN pia huondoa hofu na mtu anaanza kumzoea mtu kwa urahisi baada ya
kushiriki nae tendo la ndoa. Hivyo basi upo umuhimu mkubwa kwa mpenzi wa kweli
kukuonyesha kuwa anatoa kipaumbele kwa tendo la ndoa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni