Jumatano, 1 Novemba 2017

DALILI ZA MPENZI ASIE MWAMINIFU




                        DALILI YA MPENZI ASIE MWAMINIFU

 Ndoa nyingi sana zina vunjika, wapenzi ambao kwa muda mrefu walionekana kupendana wanafikia mahali wanaumizana kwa maneno na matendo. Kwa nini mambo haya yanatokea? Sio rahisi kuelezea kwa nini watu wanasalitiana na kuumizana. Hata hivyo haileti raha kufikiria juu ya mtu unayempenda sana kubadilika na kukusaliti. Bila shaka kila mtu anapenda awe na uhusiano ambao unamletea raha na wa kujivunia, uhusiano ambao jambo la kuaminiana ni jambo la msingi kabisa. Lakini pamoja na juhudi zetu zote ni  wazi kabisa kuwa ndoa nyingi na mahusiano mengi kati ya mwanaume na mwanamke  hayako katika hali iletayo furaha na shangwe,  mara nyingi katika mahusiano mengi uongo, ulaghai na usiri umetawala. Ulaghai hutokea pale ambapo mtu anajifanya amefuata sheria lakini kwa siri anavunja sheria. Ulaghai ni jambo ambalo linatumika na watu wote wanapotaka kuiba penzi nje ya ndoa.

Zifuatazo ni njia ambazo ulaghai unatokea:
Fikiria kuwa hivi karibuni umefunga ndoa na baada ya miezi  miwili mkeo  anaondoka na  kwenda kuhudhuria mazishi ya shangazi yake, Jumamosi ifuatiayo uko nyumbani na kujiona mpweke sana na kuamua kwenda kwenye majumba ya starehe na marafiki wa kazini kwako. Japokuwa ulikuwa hukupanga unajikuta umekunywa pombe na kupata ujasiri wa kutongoza moja kati ya wasichana uliowakuta huko. Japokuwa ni kweli unampenda sana mke wako siku hiyo unajikuta unaondoka na dada alie mrembo zaidi ya mkeo na kumpeleka Gesti house. Siku ifuatayo mkeo anakupigia simu na kuuliza akitaka kujua Jumamosi ilikwendaje kwani amepewa habari kuwa hukuwepo nyumbani saa 3 za usiku. Kuna njia tatu za kukabili swali hilo toka kwa mkeo.

(1)     KUSEMA UKWELI
“Nilijisikia upweke sana na nikaenda na George Boji na Amanda kwenye disco. Naona nilikunywa kupita kiasi na nikavutiwa na demu moja na nikavunja amri ya sita, nikazini”.Hili sio rahisi kutokea utajaribu kumueleza mkeo kuwa ulifuata sheria na kutozini na kumbe ulizini.

(2)   UONGO KAMILI
Nilikaa nyumbani na kuangalia TV hadi saa 2 na nikaenda kulala na sikusikia hodi yoyote.

(3) UKWELI USIO KAMILIKA
“Nilijisikia upweke na George Boji aliponiomba niende nae Capri cabana nilienda na kurudi saa sita. Hapa unasema ukweli lakini ukweli ambao haukukamilika, unaondoa jambo kubwa katika maneno yako. Mkeo anaamua kuwa uliosema ni kweli kumbe kuna jambo uliloficha. Japokuwa hakuna mtu anayestahili kudanganywa au kulaghaiwa ni vyema kukumbuka kuwa kila  mtu anawajibika kuwa mkweli kabisa, Ni watu wa chache ambao wanaweza kudhamiria kabisa kusema uongo na kuwaumiza wengine, watasema uongo  au kutumia  ulaghai kwa sababu ni waoga au  hawapendi malumbano  na hivyo hutumia uongo kujiepusha.


Mwanaume au mwanamke anapoiba mapenzi nje ya ndoa anazo sababu zake za kufanya hivyo na hawezi kukuambia sababu hizo. Haileti raha Kufikiria juu ya watu wapendanano kusalitiana lakini ukiwa mdadisi soma orodha ya mambo ambayo mwanaume au mwanamke angependa kuficha kama siri ya moyoni mwake.

(1)     MUDA WA KUWA PAMOJA
Mtu atasema uongo na kutoa sababu za uongo kuepuka kuwa pamoja na mwenziwe au kuonana nae. Mnaweza kuwa mmekubaliana jumamosi mwende disco na mwenzio atakutumia ujumbe akikwambia kuwa amepata wageni wa ghafla au anaenda kumuona shangazi mgojwa nk. Ataanza kuwa hapati muda wa kukaa na kuongea na wewe. Huamka na kwenda kazini bila mazungumzo ya kutosha. Akirudi toka kazini hakuna uchangamfu au mazungumzo yenye maana.

(2)     MAHUSIANO YA NYUMA
Utaambiwa uongo juu ya marafiki wa kike au wa kiume wa zamani tulikuwa marafiki tu wala hatujafanya mapenzi”. “Yule alikuwa hafai, nakupenda wewe zaidi” nk.

(3)     MIKUTANO YA SIRI
Utadanganywa juu ya muda ambao mwenzio alikuwa na mtu fulani, utaambiwa walikutana kwa bahati mbaya na walikuwa hawakupanga kukutana au walikuwa na maongezi ya kikazi, au maandalizi ya arusi n.k.

(4)     MICHEZO AU UTANI  NA WATU WA JINSIA TOFAUTI
Unapomkamata akicheza au kutaniana na mtu  mwingine wa jinsia tofauti na yake atakuambia  hakuna lolote la kimapenzi. Katika uhusiano wao. Michezo au utani wa namna hii anakuwa anao hata katika maongezi ya simuu.

(5)     HISIA, MVUTO NA KUPENDEZWA
Utadanganywa juu ya hisia zake juu ya mtu mwingine hasa wapenzi wa zamani au wafanyakazi wengine, utaambiwa kuwa hakuna uhusiano wa kimapenzi. Uonapo hali ya uchangamfu mkubwa anapokuwepo mtu wa jinsia tofauti na yake hapo inakubidi ufungue macho sawasawa.

(6)     TENDO LA NDOA
Utadanganywa kuwa wewe unajua zaidi ya wengine, utasifiwa hata kama hustahahili sifa. Tafuta ukweli halisi kadri mnavyoendelea katika mahusiano yenu, iwapo sifa zitaendelea siku zote basi sifa hizo zitakuwa za kweli. Utafiti uliofanyika na wataalamu wa sayansi ya mapenzi unaonesha karibu asilimia 70 ya wanawake hujifanya wameridhisha kumbe hamna lolote.




(7)     HISTORIA YA WAPENZI
Utadanganywa juu ya idadi ya wapenzi waliokutangulia, vitu ambavyo alifanya na wapenzi hao wa zamani. Ataanza kuwa na tabia ya kuongea na wapenzi wa zamani au kuzungumza juu yao. Kama haachi kuzungumzia juu ya wapenzi wa zamani hiyo ni dalili mbaya katika uhusiano wenu. Jiulize ni sababu gani inayomfanya akumbuke na kuanza kuzungumzia wapenzi wa zamani? Kama ameanza kukulinganisha na mpenzi wa zamani basi huenda ameanza pia kufikiria kukuacha au kutokuwa mwaminifu.

Mwanzo wa dalili za wizi wa mapenzi

Kitakuwepo kipindi Fulani ambapo mwenzio ataanzakuiba mapenzi na dalili ya haraka kuonekana ni mabadiliko ya ghafla, mabadiliko kati ya jinsi ambavyo zamani alikuwa akienenda na vile alivyo zoea kuenenda katika mahusiano yenu. Mabadiliko ya ghafla siku zote yanasababishwa na kitu fulani kipya, uonapo hilo anza kufanya uchunguzi. Kwa kuangalia yafuatayo:-

(1)      Wezi wengi wa mapenzi huonyesha dalili ambazo hata wao wenyewe hawawezi kujua na hivyo hawawezi kuzificha.
(2)      Watu wengi hawaoni au kutoa tafsiri tofauti ya dalili za wizi wa mapenzi    japo kuwa ziko wazi kwa kuwa hawazijui.
(3)      Ukifahamu  kitu cha kutafuta unaweza  kupata  dalili nyingi  za wizi wa  mapenzi kwa kutumia  macho yako, masikio yako na ufahamu ulionao juu ya mpenzi wako.
(4)      Sio dalili za wazi, ni dalili za ndanindani ambazo zinaweza kabisa kumuumbua mwizi wa mapenzi.
(5)      Ni vizuri zaidi uweze kuzigundua dalili za wizi wa mapenzi ili kuokoa ndoa yako au uhusiano wako ukichelewa unaweza kuwa umechelewa kabisa na uhusiano wako kufa.

Mpenzi wako anapo kosa uaminifu inaumiza sana  na mara nyingi huleta chuki, mawazo mabaya  juu ya mtu ambaye ulimpenda na kumwamini  kabisa, Mwanamke au mwanaume anapoiba penzi nje ya ndoa inakufanya uanze kujiuliza ni kitu gani ambacho mimi nimepungukiwa hata mwenzangu aende kuiba penzi nje ya  uhusiano wetu? Unapata shida kutafuta ni kosa gani ulilofanya ambalo limempa mwenzio sababu ya kukusaliti. Utajiuliza sasa nifanye nini?

Nafasi za mtu kuweza kuvunja uaminifu ni nyingi mno hivyo usijidanganye kwa kufikiri kuwa mke wako, mume wako kamwe hawezi kujaribiwa kufanya mapenzi na mtu mwingine.Ni kweli kwamba wanaume ndio wanaongoza katika wizi wa mapenzi lakini uchunguzi nilio fanya kwa miaka mitatu umenithibitishia kuwa wanawake nao hawako mbali sana kuwafikia wanaume. Hebu angalia jinsi idadi ya baa zenye Guest House na idadi ya Guest House zinavyoongezeka kila kona ya mji. Nimeongea na madereva wa tax na wao pia wamenithibitishia ya kwamba wanawake walioolewa nao wanajua kucheza mchezo wa kuiba penzi nje ya ndoa. Katika uchunguzi wangu nimegundua kuwa wanawake ni waangalifu sana katika kuiba penzi kuliko wanaume

Ili uweze kumkamata mwizi wa mapenzi huhitaji kwenda chuo cha polisi na upelelezi na jarida hili limeandaliwa kukusaidia uweze kugundua dalili  za mwizi mapema kabisa  kabla  mambo hayaja fika mbali, uhai na uzuri wa ndoa yako unategemea sana uwezo  wako na maarifa  ya kuweza kuzitambua  dalili za mwizi wa penzi. Zifuatazo ni dalili muhimu za kuangalia.

(1)    KUJALI SANA JINSI ANAVYOONEKANA
Mtu ambaye ameanza kuiba mapenzi nje ya ndoa utamgundua kwa kurudisha tabia za mwanzoni mwa uhusiano wenu. Ataanza kuvaa nguo za kupendeza zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida ili kumvuta vizuri mpenzi mpya, kama ni mwanamke utaona mitindo ya nywele, perfume na upambaji ghafla umeongezeka nguvu na kasi. Angalia mabadiliko haya katika nguo za kawaida hadi nguo za ndani. Kama mabadiliko ya usafi na uvaaji yameanza ghafla basi huenda mabadiliko hayo sio kwa ajili yako bali mpenzi mpya.

(2)   JINSI ANAVYO KAA NA WEWE
Uhusiano wake na mpenzi mpya utamfanya akuone wewe kuwa tishio la kufa kwa uhusiano huo wenye nguvu ya penzi jipya linalong’ara. Anakuwa mwepesi sana kukasirika, kugombana mara kwa mara. Hali hii ya kutoelewana anaifanya iwe sababu ya kuhalalisha wizi wa penzi nje ya ndoa. Ataanza tabia za kutopenda kwenda nawe katika maeneo ya starehe na kuwa na visingizio vya kumfanya asikae nawe.

(3)    ISHARA ZA MAZUNGUMZO
Vitu ambavyo mwenzio anachagua au kukataa kuzungumzia ni ishara kuwa kuna jambo la kufichwa, katika mazungumzo, anaweza kutaja majina ya watu wapya kwako, maeneo au hoteli mpya ambazo wewe na yeye hamjawahi kwenda, maeneo na vitu ambavyo kwa kawaida alikuwa akipenda kuzungumzia vinapotea katika mazungumzo yenu.

(4)   TABIA ZA KIKAZI
Kazi za ofisini ni kisingizio kikubwa  kwa mwizi wa mapenzi, hii  humpa muda wa kufanya madhambi  yake na kuchelewa kurudi nyumbani ,au kutokaa nyumbani, mara nyingi atakuwa anakwepa kukaa nyumbani kwa visingizio vya kuwa na marafiki zake wa kazini. Atakuwa hapendi ufike kazini kwake kwa kuwa unaweza kumkuta na mtu katika hali ambayo haionyeshi urafiki wa kawaida.

(5)   ZAWADI
Kuwa macho kipindi cha siku za wapendanao na sikukuu nyingine ambazo watu hupeana zawadi. Utaweza kugundua kadi au zawadi zilizofichwa maeneo ambayo anadhani huwezi kugundua. Mara nyingi zawadi hizo ni za wapenzi wake wa ziada. Pia uonapo unapewa zawadi za ghafla na za thamani kitu ambacho hakikuwa cha kawaida kwake kufanya basi zawadi hizo lengo lake ni kukufumba macho, masikio na mdomo pia. Lengo la zawadi hizi ni kukufanya uamini wewe uko peke yako na hivyo kupuuzia dalili za wizi wake.




(6)   TENDO LA NDOA
Kuwa macho uonapo kuwa mnafanya tendo hilo mara chache kuliko kawaida na pia inawezekana ghafla ukaona mnafanya tendo la ndoa mara nyingi zaidi kuliko kawaida, inapokuwa mara nyingi inamaanisha kuwa wewe umekuwa uwanja wa mazoezi ili aweze kufanya vizuri zaidi kwa mpenzi mpya, au mpenzi mpya ameweza kumrudhishia hamu ya tendo hilo na hivyo anawatumia nyote wawili kama faida yake ili ajione kuwa yye ni mtemi.

(7)   KUJIENGUA
Ataanza kuonyesha kutopenda kuwa pamoja na familia yako au marafiki zako kwa hofu kuwa huenda wakawa wamemuona katika maeneo mabaya na hivyo kukupa wewe taarifa. Anapata shida kuonyesha kuwa anakupenda au kukujali mbele za ndugu zako au marafiki zako na hivyo atatafuta sababu za kukwepa kuwa nao kwa muda mrefu. Na kama akikubali atakuwa sio mchangamfu na huenda akasisitiza muondoke mapema.

(8)   KUKWEPA MASWALI
Uonapo kuwa mwenzio anakwepa kujibu maswali fulani ambayo ni rahisi sana na ya kawaida fungua macho yako zaidi utaona makubwa au anaweza kujibu swali rahisi baada ya kuulizwa mara ya pili jambo ambalo linaonyesha alikuwa anatafuta uongo wa kukuambia. Anapoanza kusitasita kujibu maswali ambayo hapo nyuma alijibu bila kusita jua mwizi anatafuta pa kujificha.

(9)   HANA MUDA WA KUWA NAWE
Anaweza kukwambia hana muda au fedha ambazo mngeweza kutoka kwenda sehemu za burudani lakini rafiki yake akimpigia simu haraka sana atatoka. Na aondokapo atakwenda kwa muda mrefu na akirudi ukitaka maelezo anakuwa mkali au anatoa maelezo mafupi sana. Anaanza kuwa mchelewaji na ghafla anaweza kutoa sababu za kutaka atoke na muda wa kurudi kwake huwezi kutabiri.

(10)   MATUMIZI YA SIMU
Mwanaume au mwanamke ambaye ni mwizi wa mapenzi anakuwa na mabadiliko ya wazi katika matumizi ya simu yake ya mkononi.  Utaona kwamba mara kadhaa anashindwa  kupokea simu na kuongea mbele  yako au  anakuwa na wasiwasi mara simu ya  mpenzi wake inapoingia, utaona kuwa simu yake siku hizi haitoi mlio kabisa bali mitikisiko  (Vibrations), ukimpigia utaona inachukua muda mrefu kupokea simu  kuliko kawaida  au  unapomkosa  na unajua ataona MISSED CALL inachukua muda mrefu  kukupigia na kuuliza ulikuwa unahitaji  nini. Anapopokea simu ya mpenzi wake  na wewe uko nyumbani au karibu utamsikia akiongea kwa sauti ya chini sana kuliko ilivyo kawaida, maongezi  ya minong’ono  ni  dalili kuwa kuna jambo la kuficha, kama hakuna  jambo  la kuficha kwanini aongee kwa sauti ya chini ? Au kwa nini asikuruhusu ushike simu yake kama hana jambo la kuficha? Anapokuwa anaongea na mpenzi wake mpya na wewe ukaingia ghafla  utaona anakata simu haraka au anafupisha maongezi na kuaga, unapouliza alikuwa anaongea na nani anakuwa mkali au anaongea manenao ya kukwepesha au kuleta maongezi tofauti kabisa.Ukiwa unaouwezo wa kushika simu yake na kuitumia basi kagua simu zilizopigwa katika masaa ya ajabu au simu ambazo zilichukua muda mrefu katika maongezi, zifuatilie namba hizo kwa makini, na uonapo zinarudiwa rudiwa  basi anza kujua kwamba mwenzio huenda amepata mpenzi mpya. Mwanamke au mwanaume anayeiba mapenzi atakuwa na tabia ya kufuta rekodi zote za meseji (sms), namba alizozipiga au namba alizopokea, uonapo mara nyingi simu yake iko tupu tambua ya kuwa kuna siri ambayo hataki kabisa wewe uweze kuijua.

(11)   RATIBA YA KILA SIKU
Mwanamke au mwanaume aliyeanza kuiba mapenzi ataanza kuulizia juu ya ratiba yako ya kila siku.Atafanya hivyo ili aweze kumpangia mpenzi wake mpya ratiba ambayo haitakupa wasiwasi, uonapo hili basigundua kwamba anakupa nafasi ya kumtega ili uweze kumkamata.

UKAMATAJI WA MWIZI


FANYA KAZI YA ZIADA: Weka rekodi ya kila kitu anachosema ambacho kinaleta wasiwasi, weka rekodi ya siku, tarehe muda na mambo uyagunduayo. Tunza taarifa hizi ili uweze kuwa na risasi za kutosha siku ya mapambano na mwizi huyu. Itachukua muda lakini matokeo yake yatakufariji kuwa kazi yako haikuwa ya bure. Zaidi ya yote taarifa nyingi hupata nguvu zaidi unapokuwa na taarifa nyingi za zamani ambazo zinafanana na hizi mpya. Hakikisha kuwa mwenza hajui wala kuhisi kuwa unamchunguza.

FUATILIA MAMBO: Kama alisema  alichelewa  sehemu fulani, ngojea siku mbili zipite halafu muulize kuhusiana na  yale aliokueleza mwanzoni, ukiona maelezo  yanatofautiana jua ulidanganywa, Uliza watu aliokuwa nao, marafiki zake, kuwa mwangalifu  unapotaka maelezo, toka kwa  watu  wengine, Ukiona marafiki zake au wafanyakazi wenzake hawaelewi unachouliza andika hali hiyo ya wasiwasi kwa kumbukumbu ya kukusaidia baadaye.

Usiwaamini marafiki zake mia kwa mia, marafiki zake wanaweza kutumiwa kuwa ngome ya kuficha siri zake. Kwa mfano, anaposema alikuwa mahali flani  na rafiki  yake ,tafuta muda ukiwa  peke yako na mpigie simu huyo rafiki yake na kumuuliza “Vipi ilikuwaje siku ile  walipoenda ZEZE HOTEL, walikuwa  wangapi, mambo yalikuwa shangwe au vipi?” kama  marafiki  zake wanasita sita au wanakuwa wanaonekana kama hawajui la kusema jua kuwa ulidanganywa.

KUAMINI NA HATARI ZAKE
Watu wengi wanapendelea sana kuamini kuwa wake zao au waume zao hawawezi  kwenda nje ya ndoa au  nje ya uhusiano wao na hivyo  kuamini  kile kinachosemwa. Kumwamini  mwenzio kunakufanya uwe na amani na kunafariji pale usikiapo  wake au waume wa watu wengine sio waaminifu. Mara nyingi mtu anaweza kujitahidi sana kufumbia macho dalili za wizi  wa mapenzi  kukwepa  maumivu ya kuuangalia ukweli ambao unauwezo wa kuleta maumivu, jambo hili la kufumbia macho dalili za  wizi ndio sababu kubwa inayofanya mke au mume kuwa mtu wa mwisho kujua kuwa  alikuwa anasalitiwa.

Mwizi wa mapenzi  anatumia udhaifu kwa faida yake. Mwizi  wa mapenzi  ata endelea kummweleza mpenzi wake mambo  ambayo  anapenda kusikia (kamwe mimi siwezi kufanya mapenzi  na mtu mwingine zaidi  yako. Siku zote mwizi wa mapenzi  atakuwa anaangalia kama mwenzie ameanza  kuwa na mashaka  na akigundua  kuwa ameanza  kuwa na mashaka  atabadilisha  mbinu  zake za wizi  ili kuepuka aibu ya kukamatwa. Unapotaka kumkamata mwizi wa mapenzi  jitahidi sana asigundue kuwa unamuonea mashaka, jizuie, vumilia mpaka  upate ushahidi kamili, ukikosea hapo mwenzio  ataanza  kuwa mwangalifu  zaidi  na  itakuwa  vigumu  zaidi kumkamata. Baada ya  kusema haya utaona kwamba  yote yana hasara zake kwa kuwa  yana uwezo  wa kumsaidia mwizi  wa mapenzi,  hawezi kukubali kosa kabisa kama huna ushahidi wenye nguvu  ya kutosha, mara nyingi hata  ukiwa na ushahidi wa kutosha mwizi bado atajitahidi kujitetea kuwa hana hatia.

NJIA ZA KUWEKA UKWELI WAZI

Kabla hujaweka mambo wazi ni muhimu  sana ufikirie juu ya mabadiliko  unayotaka yatokee katika uhusiano wenu kuweka mabo wazi ni vigumu  kwa kuwa unafanya kitu ambacho mwenzio anakiona kama jambo linalomletea aibu au fedheha. Ili kuweka  uwazi  vizuri bila matokeo mabaya fanya mambo yafuatayo.

(I)   CHAGUA MUDA NA SEHEMU
Fanya jambo hilo mkiwa wawili  peke yenu, mahali ambapo mtu mwingine  hawezi kusikia mazungumzo yenu. Chagua muda ambao mwenzio hakuchoka, hana haraka na ametulia, usifanye jambo hili wakati mwenzio anajiandaa kwenda kazini  au safarini.

(II)         MUANDAE MWENZIO
Kabla  ya kutoa au kueleza ushahidi wako mwambie mwenzio kuwa kuna jambo muhimu ungependa kumshirikisha na muombe atulie na asifanye au kusema kwa hasira.

(III)       ELEZEA KINAGANAGA
Jitahidi kutoa maelezo yalio wazi na ya kutosha na epuka kutumia  maneno  yenye  sura ya hukumu au kulaumu. Onyesha jinsi  ushahidi  wako ulivyo sababisha  uone kuwa  hupendwi au umesalitiwa na kuumizwa. Jizuie  usiongee kwa sauti kubwa au katika hasira ili mwenzio asione kuwa anavamiwa na kushambuliwa.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

                                    HAMU YA TENDO LA NDOA KWA WANAWAKE  Mwanamke anapojikuta amepoteza hamu ya tendo la ndoa anakuwa mzigo k...